Mwenyekiti mpya UVCCM apata mapokezi makubwa

Umoja wa Vijana  wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Dar es Salaam umefanya mapokezi ya kumpokea Mwenyekiti wao mpya Kheri James akitokea Mkoani Dodoma. 

Hafla hiyo ya kumpokea mwenyekiti Mpya wa UVCCM imefanyika katika ukumbi wa Vijana Social  hall jijini Dar es Salaam. Kheri alichaguliwa rasmi kuwa mwenyekiti Desemba 13 mwaka huu. 

Katika uchaguzi huo uliofanyika mjini Dodoma, James ameibuka  mshindi kwa kupata kura 319 kati ya 583 zilizopigwa na kumwacha kwa mbali mpinzani wake, Thobias Mwesiga aliyepata kura 127. 

Akizungumza mara baada ya mapokezi hayo Kheri alisema ni wakati wa vijana wa jumuiya hiyo kuwa ngangari katika kupambana na rushwa inayoharibu taswira ya nchi. 

"Nyie ni vijana mnatakiwa kusimama imara kuhakikisha kuwa mnapambana na rushwa, pia msiruhusu mtu anayetumia rushwa kupata wapiga kura akavuruga jumuiya yetu," amesema. 

Amesema rushwa haijengi bali rushwa itawafanya vijana kuwa wasindikizaji katika taifa. Katika hatua nyingine Katibu wa Chama cha Demokrasia na maendeleo kata ya Chanika Johnson   Edward amejiunga rasmi leo Desemba 21 na chama cha mapinduzi katika hafla hiyo.

No comments